Watoto wa Mombasa katika ziara Uingereza

Watoto 14 kutoka mjini Mombasa, Kenya, na wenye umri wa chini ya miaka 13, wamekuwa nchini Uingereza kushiriki katika mechi kadhaa za kandanda.

Image caption Watoto wakiwa na makocha wao na mwakilishi wa Touraid

Kundi hilo la watoto kwa jina Coastal Kings, yaani Wafalme wa Pwani, liliweza kupambana katika soka na watoto wa shule ya Uingereza ya Elstree.

Katika kipindi cha wiki moja, watoto hao waliweza kupata jumla ya magoli tisa, na muhimu zaidi, kupata marafiki watakaodumu katika maisha yao yote.

Vijana hao waliweza kutoka sare katika mechi tatu, na kupata ushindi katika moja.

Mwalimu mkuu wa shule ya Elstree, Mark Sayer, alisema alipendezwa mno na namna vijana hao kwa upesi walivyoweza kujumuika katika jamii ya Elstree.

Mara tu walipofika walishangazwa na maisha ya Elstree, lakini baada ya muda mfupi tu, waliweza kwa ujasiri mkubwa kuyazoea masiha ya Elstree.

Mwalimu mkuu Sayer alisema itakuwa ni kwa masikitiko makubwa watasema kwaheri, wakati ukiwadia wa watoto hao kufunga safari kurudi Mombasa.

Safari ya vijana hao nchini Uingereza ilipangwa na shirika linalofahamika kama Touraid.

Kwa mengi zaidi kuhusu safari ya watoto hao Uingereza, sikiliza matangazo yetu ya Ulimwengu wa Soka, siku ya Jumamosi, yatakayoanza saa kumi unusu za Afrika Mashariki.