Newcastle yaonyesha umahiri wa soka

Kevin Nolan alifanikiwa kuifungia Newcastle magoli matatu, dhidi ya wapinzani wao kumi, timu ya Sunderland.

Image caption Newcastle ilipata mteremko ilipocheza na Sunderland

Nolan alianzisha mfululizo wa mabao, kwa kupata mawili ya kwanza.

Bao la pili liliwezekana hasa kupitia msaada kutoka kwa Andy Caroll.

Shola Ameobi alifanikiwa kuongozea bao la tatu kupitia mkwaju wa penalti, kutokana na Nedum Onuoha kumtega Jonas Gutierrez.

Mwamuzi pia hakuwa katika hali ya kumsamehe Titus Bramble, na alimuonyesha kadi nyekundu baada ya kumwangusha Caroll.

Kisha Ameobi aliweza kupata bao lake la pili, na Nolan kuongezea la tatu, kabla ya Darren Bent kupata bao la kuituliza Sunderland.

Kabla ya mechi hiyo, Aston Villa ilicheza na Birmingham City, na timu zote kugawanya pointi, kwani hakuna mabao yaliyopatikana.

Meneja Gerrard Houllier, alisikitishwa na matokeo hayo, kwani hii ilikuwa ni mara ya kwanza yeye kukutana na maadui wakubwa Birmingham, tangu achukue madaraka ya kuifundisha Villa, na alitazamia ushindi.

Katika mechi ya mwisho iliyoelekea kana kwamba pia haitakuwa na mabao, Maxi Rodriguez aliweza kufunga bao la Liverpool katika dakika ya 86, na ikichezea ugenini Bolton, kupata ushindi wa bao 1-0.

Hata hivyo Liverpool awali walikosa nafasi za wazi.

Fernando Torres hakufua dafu katika nafasi mbili za wazi kipindi cha kwanza, huku Steven Gerrard naye akikosa nafasi nzuri pia ya kuiletea timu yake fahari.

Ushindi huo ambao ni wa kwanza wa Liverpool ikicheza ugenini tangu mwezi Aprili, walipoishinda Burnley, unamaanisha sasa wamekuwa imara zaidi katika ligi ya Premier, kwani wamefanikiwa kutoka nafasi ya 18 kati ya 20, na kupanda hadi nafasi ya 12.