Liverpool yaisononesha Chelsea

Kati ya mechi tatu zilizochezwa Jumapili, Fernando Torres aliwasisimua mashabiki wengi, wakati alipofunga mabao yote, na kuishinda Chelsea magoli 2-0.

Image caption Torres alithibitisha Liverpool ina nguvu mpya sasa

Huu ulikuwa ni ushindi wa Liverpool katika mechi ya nne mfululizo, ikiwa ni pamoja na ule wa Alhamisi iliyopita, wakati iliishinda Napoli ya Italia katika ligi ya Europa.

Torres, kutoka Uhispania, kwa maarifa makubwa aliweza kuupokea mpira kutoka kwa mwenzake Dirk Kuyt, na kumkwepa mlinzi John Terry, na kuandikisha bao la mapema katika mechi hiyo.

Huku kipindi cha kwanza kikielekea kumalizika, Torres alifanya maajabu yake tena, wakati huu akipokea mpira kutoka kwa Raul Meireles, na kuupinda mpira, kufuatia kosa la Ashley Cole, na hivyo basi kuandikisha bao la pili.

Ilikuwa nusra Kuyt pia kuongezea bao la tatu, huku kipa wa Liverpool Pepe Reina naye akiokoa mikwaju kutoka kwa Florent Malouda na Nicolas Anelka wa timu ya Chelsea, lakini mchezo ulikwisha kwa magoli hayo mawili.

Licha ya kipigo hicho, Chelsea bado inaongoza ligi kufikia sasa ikiwa na pointi 25.

Katika mechi nyingine ya kusisimua kati ya Arsenal na Newcastle, wenyeji katika uwanja wao wa Imarati walifungwa goli 1-0.

Bao hilo la pekee katika mechi hiyo lilifungwa na Andy Carroll, kupitia kichezwa.

Huu ulikuwa ni ushindi wa kwanza wa Newcastle katika uwanja wa Arsenal, tangu mwezi Desemba mwaka 2001.

Manchester City nao baada ya kuboronga katika mechi za hivi karibuni, Jumapili waliweza kuwathibitishia mashabiki ni kwa nini walimsajili Mario Balotelli msimuu huu.

Wakiwa ugenini dhidi ya West Brom, Balotelli aliweza kufunga magoli mawili, na kuandikisha ushindi wa magoli 2-0.

Lakini licha ya kufunga magoli hayo, mchezaji huyo kutoka Italia alionyeshwa kadi nyekundu kwa kucheza vibaya, na timu yake ikamaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji kumi uwanjani.

Balotelli, katika kipindi cha pili, alimpiga teke Youssuf Mulumbu, muda mfupi baada ya mwamuzi kutoa onyo kali.