Mchague mchezaji mahiri wa soka Afrika

Shiriki katika shughuli ya kumchagua mchezaji bora zaidi wa soka barani Afrika, na atakayepata tuzo ya BBC ya mwaka 2010.

Wachezaji watano wanaowania tuzo hiyo ni Asamoah Gyan, Andre 'Dede' Ayew, Samuel Eto'o, Yaya Toure na Didier Drogba.

Image caption Ungana na mashabiki katika kumchagua mchezaji mahiri wa soka barani Afrika

Una nafasi ya kuamua bingwa atakuwa nani, kati ya sasa hadi tarehe 10 mwezi Disemba, na mshindi atatangazwa wiki moja baada ya hapo, Ijumaa ya tarehe 17 mwezi Desemba, katika matangazo ya moja kwa moja ya michezo kwa lugha ya Kiingereza, Fast Track, saa 1600 GMT.

Hili ni tuzo la pekee linalosifika na ambalo hutoa nafasi kwa wewe kama shabiki kuamua mshindi.

Wachezaji hao watano wanaowania tuzo waliteuliwa na wadau wa soka kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

Mshindi wa mwaka jana alikuwa ni mshambulizi wa Chelsea, Didier Drogba, na ambaye pia huichezea timu ya taifa ya Ivory Coast.

Washindi wa miaka iliyopita ni:

2009 - Didier Drogba

2008 - Mohamed Aboutrika

2007 - Emmanuel Adebayor

2006 - Michael Essien

2005 - Mohamed Barakat

2004 - Jay Jay Okocha

2003 - Jay Jay Okocha

2002 - El Hadji Diouf

2001 - Sammy Kuffour

2000 - Patrick Mboma

Baadhi ya masharti ya kumchagua mchezaji soka bora zaidi barani Afrika mwaka 2010

Ni nani anafaa kuchaguliwa?

Mchezaji yeyote anayeichezea timu ya taifa ya Afrika anaruhusiwa kuwania tuzo ya BBC ya mchezaji bora zaidi barani Afirka.

Kura ya Umma

Kufuatia kutangazwa kwa orodha ya walioteuliwa kuwania tuzo, mshindi atachaguliwa kwa kura kutoka kwa umma.

Unaweza kushiriki kwa kupiga kura kupitia mtandao, au kwa kuandika ujumbe wa SMC.

Shughuli ya upigaji kura itaanza saa 1700 GMT, Jumatatu, tarehe 17 Novemba, na itafungwa saa 1700 GMT, Ijumaa, tarehe 10 Desemba 2010.

Kura za mtandao na zile za ujumbe wa SMS zitachanganywa na kuhesabiwa pamoja, na matokeo ya mshindi yatapatikana katika tovuti ya 'BBC African Fooballer of the Year', ambao pia ina masharti mbalimbali na vikwazo vyote vya kushiriki katika upigaji kura.