Nigeria ni mabingwa tena katika soka

Nigeria ilifanikiwa kuwa bingwa wa mashindano ya kina dada ya soka barani Afrika, baada ya kuwashinda mabingwa watetezi Equatorial Guinea magoli 4-2 siku ya Jumapili, nchini Afrika Kusini.

Mabao ya dakika za mwishomwisho yaliiwezesha Super Falcons kutwaa ushindi wao wa sita.

Licha ya mchezo mzuri, kina dada kutoka Guinea walijiangamiza kwa kujifunga wenyewe mara mbili, na kupoteza matumaini ya kuhifadhi ubingwa.

Image caption Equatorial Guinea imeshindwa kuutetea ubingwa wake wa Afrika

Mchezaji aliyeandikisha magoli mengi zaidi katika mashindano, Perpetua Nkwocha, aliiwezesha Nigeria kuongoza baada ya dakika saba za mchezo.

Bao la Super Falcons liliwazindua Equatorial Guinea, na walianza kucheza kwa makini zaidi na Carolina Parreira kusawazisha katika dakika ya 66.

Ugochi Oparanozie aliweza kuiwezesha Nigeria kuongoza tena, baada ya dakika 11, kupitia bao la kichwa.

Super Falcons waliendelea kuumiliki mchezo vyema, wakati Ghislaine Nke alimfunga mlinda lango wake mwenyewe, na kuwasaidia Nigeria kuongoza kwa magoli 3-1.

Baadaye, Jada Sayo aliifanya Equatorial Guinea kuwa na matumaini baada ya kuandikisha bao, lakini Parreira alipofunga bao dhidi ya kipa wake mwenyewe, Nigeria wakaibuka washindi.

Timu hizo mbili ambazo zimeongoza katika mashindano hayo, zitaliwakilisha bara la Afrika katika mashindano ya kina dada ya Kombe la Dunia nchini Ujerumani, na yatakayofanyika mwaka ujao.