Chelsea yachapwa nyumbani

Asamoah Gyan
Image caption Gyan alifunga kwa ustaadi

Mabingwa watetezi wa Ligi ya Premier ya England Chelsea wamefungwa bila ubishi kwenye uwanja wao wa Stamford Bridge na Sunderland.

Beki wa Chelsea Branislav Ivanovic aliponea chupuchupu adhabu ya kadi nyekundu kwa kumtega Danny Welbeck lakini Nedum Onuoha akipita eneo hilo hilo aliwazungusha Mabeki watatu pamoja na kipa kuipatia Sunderland bao la kwanza.

Baada ya mapumziko Sunderland ikiongoza bao 1-0 katika mchezo wa kugongeana Asamoah Gyan akasuka mpira mzuri uliomgaragaza Petr Check na kuipa Sunderland matumaini ya ushindi mnono kwenye uwanja wa Chelsea.

Makosa ya hapa na pale ya wachezaji wa Chelsea yalidhihirika Ashley Cole alipojaribu kuokoa hatari iliyomkaribia kwa kutoa pasi iliyogeuka zawadi kwa Welbeck akiipatia Sunderland ushindi wa kishindo dhidi ya Klabu iliyojiwekea sifa ya kutofungwa nyumbani.

Kasi, gonga na kujiamini kwa washambuliaji Gyan na Welbeck pamoja na Mabeki waliosimama imara ndiyo nguvu iliyoiwezesha Sunderland kuipa kichapo Chelsea na kuikosesha pointi tatu.