FIFA yasimamisha maofisa

Shirikisho linalotawala mchezo wa mpira wa miguu duniani,FIFA limewasimamisha wanakamati wake 2 baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka kanuni za shirika hilo za nidhamu.

Image caption Amos Adamu wa Nigeria asimamishwa na FIFA

Amos Adamu kutoka Nigeria na Reynauld Temari mjumbe kutoka Tahiti waligunduliwa na gazeti la Uingereza wakijadili uwezekano wa kuuza kura zao za kuandaa fainali za Kombe la Dunia la mwaka 2018 na 2022 ili wanufaike kwa kuwekeza katika miradi yao binafsi.

Amos Adamu amesimamishwa kushiriki mchezo wa mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka mitatu, na mwenzake Reynauld Temari mwaka mmoja. Wote hawatoshiriki kura itakayopigwa mwezi ujao kuamua ni nchi zipi zitakazoandaa fainali mbili zijazo za Kombe la Dunia.

Gazeti la Sunday Times la hapa Uingereza lilimkuta Adamu akijadili utayarifu wake kubadilishana kura yake na viwanja bandia vilivyotengenezwa kwa plastiki.

Alitaka apokee pesa hizo mwenyewe. Mwenzake Temari alitaka ziwekezwe katika akademi ya michezo nchini mwake. Wengine wanne waliogunduliwa na gazeti hilo ni vigogo wa zamani kwenye Kamati kuu ambao nao wamesimamishwa, ingawa FIFA haijatoa maelezo kamili kuwahusu.

Kamati ya maadili ya FIFA hata hivyo haikupata ushahidi wa kutosha kuhusu madai ya ushirikiano wa Uhispania na Ureno kutaka njia ya mkato ili kuandaa fainali ya mwaka 2018 pamoja na Qatar kuandaa fainali za mwaka 2022 hayakuthibitishwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya maadili ameshutumu jinsi gazeti la Sunday Times lilivoendesha upelelezi wake, akidai kuwa gazeti hilo liligeuza ukweli ingawa alisema hatua iliyochukuliwa dhidi ya wahusika ni kunusuru mchezo wa mpira wa miguu kwa ujumla.