Hughes ashindwa kulipiza kisasi

Meneja wa zamani wa Manchester City, Mark Hughes, Jumapili alishindwa kulipiza kisasi dhidi ya timu iliyomfuta kazi mwezi Desemba mwaka jana, wakati alipoiongoza timu ya Fulham katika kuwakaribisha wageni katika uwanja wa Craven Cottage, na waliowafunga wenyeji magoli 4-1.

Image caption Mark Hughes

Matatizo ya Fulham yalianza mapema, wakati Chris Baird alishindwa kuondoa mpira hatarini, na kuupiga hadi kwa Gareth Barry, ambaye pasipo kuchelewa, alimfikishia Carlos Tevez, na aliyefanikiwa kuandikisha bao la kwanza katika mechi, kwa mkwaju wa chini kwa chini, ambao kipa Mark Schwarzer hakuweza kuona chochote.

Bao la pili la Man City lilifungwa na Pablo Zabaleta, katika dakika ya 32.

Mechi hiyo iliekea bila shaka kuwa ni mteremko kabisa, kwani hata kabla ya mashabiki wa Man City kukamilisha sherehe za kushangilia bao hilo, Gnegneri Toure Yaya aliweza kufunga bao katika dakika ya 35.

Katika kipindi cha pili, Carlos Tevez aliweza kuthibitisha umahiri wake tena, alipoandikisha bao la nne katika dakika ya 56.

Image caption Maradona alitizama wachezaji wawili wa Argentina wakifunga mabao Craven Cottage

Ilikuwa ni fahari kwa Tevez, kwani kocha wake wa zamani katika timu ya taifa ya Argentina, Diega Maradona, na aliyekuwa amealikwa na Fulham, aliweza kumtizama akifunga bao la kwanza na la nne la City.

Man City walielekea walihitaji mabao mengi, licha ya kwamba meneja Hughes alikuwa amefanya mabadiliko katika timu yake ya Fulham, akimruhusu Zoltan Gera kuinga badala ya Damien Duff.

Ingawa Fulham waliongeza juhudi, huku mchezaji wa zamani wa City, Dickson Etuhu akionyeshwa kadi ya manjano, ilikuwa vigumu kwa Fulham kupata mabao.

Lakini zikiwa zimesalia dakika 20 mechi kumalizika, bila shaka wachezaji wa Fulham hawakutaka aibu kiasi hicho katika kushindwa wakiwa nyumbani, na Zoltan Gera alipata bao la kufutia machozi, au pengine kero za kufungwa, kwa kuandikisha bao lao la kwanza.

Hata hivyo Manchester City walikuwa wamekusudia kufanya kazi yao sawasawa, wakifahamu ushindi ungeliwawezesha kupunguza pointi kati yao na Chelsea ambao wanaongoza ligi, tofauti ikiwa ni pointi tatu tu.

Chelsea wanaongoza ligi wakiwa na pointi 28, na Man City sasa wamo katika nafasi ya nne, wakiwa na pointi 25.