Sunderland yaivisha sanda West Ham

Asamoah Gyan na Jordan Henderson
Image caption Bao la Jordan limeirusha Sunderland hadi nafasi ya saba ligi ya Premier

Goli moja ambalo lilipatikana kupitia juhudi za Jordan Henderson lilitosha kuendelea kuhakikisha Sunderland wanawaongezea majonzi West Ham, na kuhakikisha wanawaongezea kazi ya kujiondoa kutoka nafasi ya mwisho katika ligi ya Premier.

Mchezaji wa Ghana Asamoah Gyan aliweza kumpitishia kiungo cha kati Henderson mpira, na pasipo kuchelewa, kupiga mkwaju wa kasi ambao mlinda lango wa West Ham, Robert Green, alihisi upepo tu mpira ulipompita.

Bao hilo pia liliiwezesha Sunderland kuhifadhi rekodi yao nzuri ya kutofungwa katika uwanja wao wa nyumbani, licha ya West Ham kushambulia kwa dhati katika juhudi za kusawazisha.

Ushindi huo umeweza kuifikisha Sunderland katika nafasi ya saba, ilhali 'Hammers', yaani nyundo, kama wanavyojulikana West Ham, pasipo ubishi, wanavuta mkia.

Ingawa West Ham ina pointi 12 sawa na Wolverhampton, wao bila kuionea haya nafasi hiyo, wamejipata katika hali hiyo kwa kuwa wana magoli machache zaidi.