Blatter kuitakasa FIFA

Rais wa FIFA anataka kamati ya kupambana na ufisadi
Image caption Sepp Blatter

Rais wa shirikisho la kimataifa la soka, FIFA, Sepp Blatter, amesema atalifikiria zaidi wazo la kuanzisha tume ya kupambana na ufisadi katika shirikisho hilo, kufuatia malalamiko ya ufisadi hivi karibuni, madai dhidi ya baadhi ya wajumbe wa shirikisho hilo.

Blatter, akizungumza na mwandishi wa gazeti la Uswisi, (Sonntag Zeitung) alisema atatoa pendekezo hilo katika mkutano ujao mkuu wa shirikisho la FIFA, ambao unatazamiwa kufanyika mjini Zurich, mwezi wa Juni.

Alisema maafisa wakuu wa kamati hiyo itakukwa ni baadhi ya watu maarufu katika michezo, wanasiasa, wafanyibiashara, na watu wengine mbalimbali wanaohusika na masuala ya utamaduni.

Mwezi Oktoba mwaka jana, FIFA iliwasitisha wajumbe wawili katika shughuli zao katika shirikisho hilo, kufuatia madai kwamba walikuwa wana mipango ya kupokea senti, kabla ya kuamua kura yao ya kuichagua nchi itakayokuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia, mwenyeji wa mashindano ya 2018, na vile vile mwaka 2022.

Wajumbe wote wawili walikanusha madai hayo.