Hodgson atoa mwito kwa Liverpool

Hodgson (kushoto) na Ferguson
Image caption Hodgson ana matumaini ya kuitimua Man U kutoka Kombe la FA

Kocha wa Liverpool, Roy Hodgson, ambaye mambo yamekuwa yakimwendea mrama katika mechi chache zilizopita, amewataka wachezaji wake kuonyesha maarifa yao yote siku ya Jumapili, na kuiondoa Manchester United kutoka Kombe la FA, katika mechi ya raundi ya tatu siku ya Jumapili.

Liverpool itakuwa ni mwenyeji wa Man U katika uwanja wa Old Trafford.

"Mechi hii ya hali ya juu itakuwa ni nafasi nzuri kwa sisi kuweza kusahau yaliyopita baada ya kushindwa na Blackburn", alielezea Hodgson.

"Mchezo huu dhidi ya maadui wetu wakubwa kabisa ni nafasi ya kuthibitisha sisi ni bora zaidi, kuliko ilivyojitokeza Jumatano iliyopita".

Hodgson alikuwa akizungumza kupitia matangazo ya televisheni ya klabu, baada ya Liverpool kufutilia mbali mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa.

Maafisa wa klabu walifutilia mbali mkutano huo, kama juhudi za kuvizuia vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikitaka sana kujua hatma ya kocha huyo baada ya matokeo mabovu mara kwa mara msimu huu.

Liverpool kwa hivi sasa imo katika nafasi ya 12 katika ligi kuu ya Premier ya England, na ikiwa imevuka hatua ya kushukishwa daraja kwa pointi nne tu.

Hodgson ameweza kuiongoza timu hiyo kushinda katika mechi saba peke yake, kati ya jumla ya mechi 20 alizozisimamia.

Lakini ana matumaini mambo huenda yakawa tofauti Old Trafford siku ya Jumapili.

Unaweza kufuatia mechi hizo za Kombe la FA raundi ya tatu katika matangazo yetu ya Ulimwengu wa Soka, siku ya Jumamosi, na vile vile katika Michezo na Wachezaji siku ya Jumapili.

Vile vile mwishoni mwa wiki hii tutaangazia mechi za Kombe la Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 mjini Kigali, Rwanda.