Roy Hodgson afutwa kazi

Kocha wa Liverpool, Roy Hodgson, ameondoka uwanja wa Anfield, baada ya kushauriana na tajiri anayemilikii klabu.

Image caption Roy Hodgson

Hodgson, mwenye umri wa miaka 63, alifanikiwa kupata ushindi katika mechi 20 tu za ligi ya Premier, kati ya mechi 20, tangu kuchukua madaraka hayo ya kocha kutoka kwa Rafael Benitez, mwezi Julai mwaka 2010.

Matokeo hayo mabaya yameifanya Liverpool kuteremka hadi nafasi ya 12 katika ligi kuu ya Premier.

Mchezaji wa zamani na vile vile meneja, Kenny Dalglish, atashikilia madaraka ya meneja hadi mwisho wa msimu.

"Pande zote mbili ziliafikiana kwamba kwa kuzingatia maslahi yao, ni vyema aondoke", alielezea Mmarekani anayemiliki klabu, John W Henry, kupitia maelezo katika tovuti ya klabu.

Hodgson alikataa kujibu maswali kuhusu hatma yake katika uwanja wa Anfield, baada ya Liverpool kushindwa magoli 3-1 na Blackburn, Jumatano iliyopita.

Hiyo ilikuwa ni mara ya tatu kwa Liverpool kushindwa, kati ya mechi nne za mwisho ilizocheza katika ligi kuu ya Premier, hali ambayo inaifanya kuwa salama isishuke daraja, kwa kuvuka msitari huo kwa pointi nne tu zaidi.

Wakati mkutano wa Liverpool kuzungumza na waandishi ulipofutiliwa mbali siku ya Ijumaa, kuzungumzia juu ya mechi ya Jumapili ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United, uvumi ulizuka mara moja kwamba mkataba wa kocha huyo ambaye zamani aliiongoza Fulham, ulikuwa hatarini.

Unaweza kufuatia mechi za Kombe la FA raundi ya tatu katika matangazo yetu ya Ulimwengu wa Soka, siku ya Jumamosi, na vile vile katika Michezo na Wachezaji siku ya Jumapili.

Vile vile wikendi hii tunaangazia mechi za Kombe la Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 mjini Kigali, Rwanda.