Qatar yapinga mapendekezo

Mkuu wa soka barani Asia, Mohamed Bin Hammam, amepinga mapendekezo ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar, kufanyika wakati wa majira ya baridi, badala ya majira ya joto.

Image caption Mohamed Bin Hammam

Amekataa pia pendekezo la nchi hiyo kushirikiana na mataifa mengine ya bara Asia kuandaa mashindano hayo.

Shirikisho la soka duniani, FIFA, limeelezea ili kufanya mashauri kuhusiana na mabadiliko hayo, litahitaji idhini ya chama cha soka cha Qatar, jambo ambalo Bin Hammam anasisitiza halitafanyika.

Moja kwa moja pia alitupilia mbali wazo la "Kombe la Dunia kwa mataifa ya Ghuba", kama ilivyopendekezwa na Rais wa shirikisho la soka barani Ulaya, UEFA, Michel Platini, wiki hii.

"Hayo hayatuvutii. Qatar inaweza kuandaa na kufanya yote ikiwa peke yake", alielezea.

"Sisi tuna furaha na tunatoa ahadi kwa ulimwengu, tutaandaa Kombe la Dunia la kuvutia mwezi Juni na Julai", alielezea Rais huyo wa shirikisho la soka la bara Asia, raia Qatar.

Michel Platini, ambaye yumo katika kamati ya FIFA, alikuwa alitoa maoni akisema inafaa mataifa ya Ghuba kushirikiana kuandaa mashindano ya mwaka 2022, kwa kuwa Qatar ni taifa dogo, huku Rais wa FIFA Sepp Blatter, naye awali alipendekeza mashindano yafanyika wakati wa majira ya baridi, kwa sababu mwezi wa Juni joto katika eneo hilo hupanda hadi nyuzi joto 50.

Lakini Bin Hammam, ambaye inasemekana ana nafasi nzuri zaidi ya kurithi madaraka ya Blatter, alisema wakuu hao wa soka wote walifanya kosa kuelezea mapendekezo yao waziwazi pasipo kushauriana.