Blackburn yaendelea kuwika

Nyota ya Blackburn iliendelea kung'ara, hasa kwa kuipata West Brom ambayo ni hafifu, na kuitumia nafasi hiyo kusonga hadi nafasi ya saba katika msimamo wa ligi kuu ya Premier ya England.

Kwa kuchanganyikiwa, mlinzi wa West Brom, Gabriel Tamas, aliuelekeza mpira wa kichwa katika lango lake lenyewe, kutoka mpira uliopigwa na David Dunn, katika dakika ya 41.

David Hoilett naye baadaye aliteremsha mkwaju, na mpira kumpita kwa kasi kipa Boaz Myhill, na kuandikisha bao la pili la Blackburn.

Image caption West Brom walitazamia kupata penalti kwa kuangushwa Odemwingie

Wageni kabisa hawakuwa na bahati, kwani wakati Peter Odemwingie alipoangushwa, West Brom waliruhusiwa free-kick, badala ya nafasi ya kupiga penalti.

Kiungo cha kati wa Blackburn, Jermaine Jones alimchezea vibaya mchezaji huyo wa Nigeria, na picha za televisheni zilionyesha kwamba licha ya mchezo mzuri kwa jumla, ilikuwa nusra ajiharibie mechi yake ya kwanza akiichezea Blackburn.

Wenyeji pia inafaa wamshukuru sana mlinda lango wao, Paul Robinson, kwa mikwaju aliyoweza kuiokoa timu, ikiwa ni pamoja na shuti kali mara tatu kutoka kwa Jerome Thomas, na aliyempatia kibarua kigumu Michel Salgado upande wa kushoto wa uwanja.

Meneja wa Blackburn, Steve Kean, bila shaka atafurahishwa na ushindi huo wa magoli 2-0, hasa kwa kuwaruhusu Jones na Roque Santa Cruz kuichezea klabu mechi yao ya kwanza.