Uwanja kuwa wa West Ham baada ya 2012

Klabu ya soka ya West Ham United imechaguliwa kuumiliki uwanja wa Olimpiki katika eneo la mashariki mwa jiji la London, baada ya mashindano ya Olimpiki mwaka 2012.

Wakurugenzi wa kampuni ya Olympic Park Legacy (OPLC) inayousimamia uwanja huo, waliamua kulikubali ombi la West Ham, dhidi ya wapinzani wao Tottenham Hotspur.

Haki miliki ya picha PA
Image caption West Ham sasa kuumiliki uwanja wa Olimpiki London baada ya 2012

Uamuzi huo sasa itabidi kuidhinishwa na bodi ya OPLC, idara mbili za serikali, na vile vile Meya wa London.

Hatua hiyo inatazamiwa kufanyika wiki ijayo.

Wakurugenzi wote, pasipo pingamizi, waliunga mkono uamuzi wa uwanja huo kumilikiwa na West Ham.

Mpango wa Spur ulipingwa mno kwa kuwa ni ilikuwa ni kuubomoa uwanja huo, na kujenga uwanja mkubwa na wa kisasa wa soka.

Tottenham ilikuwa na mipango ya kugharamia, kwa kuhamisha vifaa vya riadha, kutoka uwanja huo hadi uwanja wa Crystal Palace, badala ya kuendelea kuwepo kwa vifaa hivyo katika uwanja wa Olimpiki katika mtaa wa Stratford.

Kinyume na Tottenham, West Ham iliahidi kudumisha vifaa vya riadha, na kuiacha sehemu ya riadha kama ilivyojengwa, pasipo kufanya marekebisho yoyote.