Sudan tayari kwa Kombe la Afrika

Chama cha soka cha Sudan kimeelezea kwamba kina uwezo wa kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa barani Afrika.

Ufanisi wa michuano ya wachezaji wanaoshiriki katika ligi za nyumbani barani Afrika, CHAN, unamaanisha kwamba Sudan ni "tayari" kuandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, kwa mujibu wa chama hicho cha soka.

Image caption Wachezaji wa Tunisia wakishangilia ushindi wao wa CHAN

Mashindano hayo ya CHAN yaliyoshirikisha timu 16, yalikwisha Ijumaa, tarehe 25 Februari, wakati Tunisia ilipoishinda Angola magoli 3-0 katika fainali.

Yalikuwa ndio mashindano makubwa Sudan ilikuwa mwenyeji, tangu mwaka 1970.

"Nadhani tuko tayari kuandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika", alisema makamu mwenyekiti wa chama cha soka cha Sudan, Ahmed El-Sheik, akizungumza na BBC.

Alielezea kwamba katika hali ya kujiandaa kwa mashindano ya CHAN, viwanja vya soka vimekarabatiwa, na shirikisho la soka barani Afrika, CAF, lilipendezwa na namna nchi hiyo iliweza kufanikiwa kama mwenyeji.

"Tumekuwa tukiisihi serikali yetu kuimarisha miundo mbinu na viwanja, na mabadiliko makubwa yamefanyika, hasa Khartoum na Medany. Serikali yetu imewekeza fedha nyingi katika viwanja", alielezea El-Sheikh.

Dosari iliyojitokeza katika mashindano hayo ni ghasia ambazo zilijitokeza katika mechi ya nusu fainali, kati ya wenyeji dhidi ya Angola.

Sudan ilishindwa, na mashabiki kuanza kurusha mawe na chupa uwanjani, wakati wa mechi, na baada ya mechi pia.