QPR yakaribia kuingia Premier

Heidar Helguson
Image caption Helguson aisaidia QPR kukaribia kujiunga na ligi kuu ya Premier

Heidar Helgusonalifanikiwa kufunga mara mbili, wakati timu yake ya Queen Park Rangers ilipocheza na Crystal Palace, iliyokuwa na wachezaji kumi, na kuiwezesha QPR kukaribia zaidi kupanda daraja na kushiriki katika mechi za ligi kuu ya Premier ya England.

Mshambulizi Helguson aliutambariza golini mpira kutoka kwa mwenzake Adel Taarabt na kuandikisha bao la kwanza.

Wageni Crystal Palace waliweza kusawazisha katika mechi hiyo ya ligi ya Championship, wakati James Vaughan alipofanikiwa kufunga bao kwa mkwaju kutoka yadi sita.

Nahodha wa Crystal Palace, Patrick McCarthy aliamrishwa na mwamuzi kuondoka uwanjani baada ya kumvuta Taarabt katika boksi, na Helguson akaweza kutumbukiza mkwaju wa penalti.

Timu hizo zilifanya juhudi kubwa ya kujiongezea pointi, na ilikuwa mechi ya kuvutia sana katika uwanja huo wa QPR, barabara ya Loftus.

Crystal Palace walikuwa katika jitihada za kuepuka kushuka daraka, baada ya kushindwa katika mechi 12 zilizopita, huku QPR wakitazamia kuingia ligi ya Premier, na wakiwa na rekodi bora zaidi katika mechi za ligi hiyo.

Kwa hiyo haikuwa jambo la kushangaza kwamba waliweza kuwika katika kumiliki mpira kwa asilimia kubwa.

Ushindi huo umepatikana baada ya wiki iliyokuwa na matatizo mengi kwa Rangers, wakihofia wataadhibiwa kwa kupunguziwa pointi na chama cha FA, kufuatia utaratibu uliokuwa na dosari katika kumsajili Alejandro Faurlin, mwaka 2009.