Qatar 'ilihonga' kuandaa Kombe la Dunia

Jack Warner na Mohamed Bin Hammam
Image caption Warner anadai Qatar 'ilinunua' michuano ya Kombe la Dunia 2022

Makamu rais wa shirikisho la soka duniani, FIFA, Jack Warner, na ambaye amesitishwa kazi, ameitoa hadharani barua pepe ambayo inadai kwamba Mohamed Bin Hammam 'aliyanunua' mashindano ya mwaka 2022, ili nchi yake ya Qatar kupata nafasi ya kuandaa michuano ya Kombe la Dunia.

Katibu mkuu wa FIFA Jerome Valcke amekiri kuipokea barua hiyo, ambayo pia iliuliza ni kwa kigezo kipi mkuu wa soka ya Asia Bin Hammam aliruhusiwa kushindania urais wa FIFA.

Valcke aliandika: "[Hammam] alidhani unaweza kuinunua Fifa kama walivyonunua Kombe la Dunia."

Hata hivyo Valcke alielezea "ilikuwa ni barua pepe ya kibinafsi", na kudokeza kwamba Warner alikuwa amechapisha sehemu fulani tu za barua hiyo.

"Yeye [Warner] aliniandikia barua pepe akiniuliza ikiwa nataka [Bin Hammam kuwania urais wa Fifa], na alisema nimshauri Bin Hammam kujiondoa," Valcke aliongeza.

Valcke pia alikanusha kuwa na ushawishi wowote katika kamati ya FIFA ya maadili ambayo imemsitisha kazi Warner na Bin Hammam siku ya Jumapili, kutokana na madai tofauti kuhusiana na kupokea mlungula, huku uchunguzi zaidi ukiendelea.