Rais wa shirikisho la kimataifa la soka, Fifa, Sepp Blatter, amesema hana nia ya kuiadhibu FA

Sepp Blatter amesisitiza hana nia ya kuiadhibu England kutokana na juhudi za kumzuia kuchaguliwa tena pasipo kupingwa ili kuliongoza shirikisho la kimataifa Fifa kwa muhula wa miaka minne zaidi.

Image caption Asema hana ugomvi na chama cha FA

Chama cha soka cha England, FA, kilitaka uchaguzi wa Jumatano kuahirishwa, lakini uamuzi huo ulipingwa vikali na wajumbe wa Fifa waliofika katika kikao cha Zurich.

Blatter alielezea kushangazwa na hatua hiyo ya FA, lakini alisema binafsi hana ugomvi na chama hicho cha England.

"Sina kinyongo na ubaya wowote na vyama ambavyo havikunichagua", alielezea.

"Mimi ni rais wa mashirikisho yote, na nitafanya kazi kwa kushirikiana na yote - na ni fahari kupata kura 186. Msiwe na wasiwasi na Waingereza".

"Shirikisho la kimataifa nambari moja katika Fifa - FA, lilianzisha mchezo wa soka mwaka 1863 - na lina haki ya kuitwa FA, chama cha soka. Linatakikana kuwa mfano, kwa hiyo hilo lilinishangaza.

Nilikuwa nimeyasikia hayo, na Uefa lilikuwa na kikao maalum kujaribu kuwashawishi. Nilidhani tatizo hili litapata suluhu, kwa hiyo nilishangaa walipojaribu kubadilisha ajenda ya kongamano na kutofanya uchaguzi", alielezea Blatter.

Wakati huohuo, makamu rais mpya Jim Boyce ameielezea BBC kwamba chama cha FA kitahitajika kupata wakuu wapya, kwa misingi ya kuimarisha uhusiano tena kati yao na shirikisho la Fifa.