Pienaar kukosekana Misrii

Steven Pienaar, baada ya kuondoka uwanjani Alhamisi akichechemea, huenda akalikosa pambano la kufuzu la michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, wakati Afrika Kusini itakapocheza na Misri siku ya Jumapili.

Pienaar, mwenye umri wa miaka 29, alikuwa akifanya mazoezi na kikosi cha timu ya Afrika Kusini kabla ya kuelekea Cairo wakati alipoondoka uwanjani huku akiwa ameshika goti, katika uwanja wa Rand.

Image caption Inaelekea ataikosa mechi ya Cairo

Licha ya kupata usaidizi wa kimatibabu kando ya uwanja, bado kuna shaka iwapo atacheza dhidi ya Misri.

Kocha wa Bafana Bafana, Pitso Mosimane, ameelezea kwamba ana shaka ikiwa mchezaji huyo, kiungo cha kati, ataweza kushiriki katika pambano hilo la kundi G.

"Bado anachechemea", alielezea Mosmiane. "Nyote mlimtizama Steven akicheza kwa asilimia 50/50 akiwa na matumaini ya kucheza, kabla ya kujeruhiwa goti lake".

"Tuna siku mbili, kwa hiyo tutasubiri na kuona hali itakuwa vipi. Pengine maumivu yatapungua, huwezi kutabiri. Lazima nisubiri na kumsikia daktari atasema nini".

Pienaar tayari alikuwa na maumivu ya nyongo, na Jumatatu aliahirisha upasuaji, ili kwanza acheze dhidi ya timu hiyo ya Firauni mjini Cairo.