Friedel kuichezea Spurs

Mlinda lango kutoka Marekani, Brad Friedel, amekubali kujiunga na klabu ya Tottenham.

Image caption Kipa wa Villa kuichezea Tottenham

Sasa inafahamika kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40, ambaye mkataba wake na klabu ya soka ya Aston Villa ulitazamiwa kwisha mwishoni mwa mwezi huu, ametia saini mkataba wa miaka miwili na Tottenham.

Meneja wa Tottenham, Harry Redknapp amesema: "Ni vyema kuwa na walinda lango wazoefu watatu katika klabu [Heurelho] Gomes, Carlo [Cudicini] na sasa Brad.

"Inamaanisha kutakuwa na ushindani katika kuwania nafasi kucheza, hasa kutokana na mechi nyingi tunazozitazamia msimu ujao".

Friedel, ambaye atapatikana pasipo ada yoyote, ana uzoefu mkubwa katika ligi kuu ya Premier, tangu alipojiunga na Liverpool kutoka klabu ya Marekani ya Columbus Crew, Desemba mwaka 1997.

Aliweza kuichezea Liverpool katika mechi 30, kabla ya kujiunga na Blackburn, na hatimaye kucheza zaidi ya mechi 365 katika kipindi cha miaka minane.

Kisha alijiunga na Villa mwezi Julai mwaka 2008, na Desemba iliyofuata, alivunja rekodi ya mchezaji kucheza mfululizo mechi nyingi katika soka ya hali ya juu, kwa kushiriki katika mechi 167, na rekodi aliyoiendeleza kwa kufikisha mechi 275 msimu huu uliokwisha.