Mgogoro waendelea ndani ya CONCACAF

Mvutano katika mkusanyiko wa mashirikisho ya soka, CONCACAF, bado unaendelea, na kaimu rais, Lisle Austin, Jumamosi amesimamishwa kazi kwa muda, kwa kukiuka hatua kanuni fulani kuhusiana na uongozi wa shirikisho.

Afisa huyo kutoka Barbados amekuwa kaimu wa shirikisho hilo ambalo linasimamia kandanda eneo la Kaskazini, Marekani ya Kati na Caribbean, tangu kusitishwa kazi kwa Jack Warner.

Kamati ya maadili ya FIFA ilimsimamisha kazi Warner na kuamuru asishiriki katika shughuli zozote za soka, hadi uchunguzi kamili kuhusiana na madai ya kupokea mlungula umemalizika.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Blazer aliwasilisha madai ya kupokea mlungula dhidi ya rais wa CONCACAF aliyesitishwa kazi Jack Warner

Madai hayo yaliwasilishwa na mjumbe mwenzake katika kamati ya uongozi ya FIFA, Chuck Blazer.

Austin alikabidhiwa jukumu la kuiongoza CONCACAF, lakini kulingana na taarifa katika wavuti www.concacaf.com, sasa amesitishwa kazi, na afisa mmoja kutoka Honduras, Alfredo Hawit, sasa atashikilia kwa muda madaraka hayo.

Taarifa hiyo ilieleza: "CONCACAF imemsimamisha Lisle Austin kwa muda kuendesha shughuli zozote za soka, na katika katika soka ya kitaifa, kupitia uamuzi wa wengi katika kamati kuu ya CONCACAF, kufuatia kukiuka kanunui muhimu za shirikisho".

"Kama afisa wa cheo cha juu zaidi akiwa ni makamu wa rais, Alfredo Hawit, kulingana na sheria za CONCACAF, sasa atakuwa ndiye kaimu wa rais".

Austin ana nafasi ya kujitetea tarehe 13 mwezi Julai, na anaweza kukata rufaa kwa kusitishwa kazi, kabla ya tarehe 13 mwezi Juni.