McLeish ajiuzulu kama kocha Birmingham

Klabu ya Birmingham city iliyoshushwa daraja mwisho mwa msimu uliopita imetangaza kuwa Kocha wake Alex McLeish amejiuzulu kupitia barua pepe au email kwa Mwenyekiti Peter Pannu mapema leo.

Itakumbukwa kuwa McLeish alipendelewa na bodi nzima ya uongozi wa klabu ya Birmingham city licha ya kushuhwa daraja kutoka Ligi kuu ya England kwa imani kuwa ataweza kuirejesha katika kipindi cha msimu mmoja.

Wakuu wa Birmingham walitarajia kuwa uzowefu wa Kocha huyo na jinsi alivyowafahamu wachezaji angeweza kuirejesha katika Ligi kuu katika kipindi cha Msimu mmoja.

Image caption Alex McLeish

Kocha huyo amechukuwa uwamuzi bila kusukumwa wakati kuna uvumi mkali kuwa anajisafishia njia ya kuajiriwa na klabu ya Aston Villa ambayo inajitahidi kutafuta Kocha baada ya Gerrard Hollier kuondoka kwa sababu za kiafya.

Raia huyu wa Scotland alishika hatamu za kuiongoza Birmingham City kwa mara ya kwanza mwaka 2007 lakini hakuwa na dawa yoyote ya kuiepusha na mkasi wa kushuka daraja.

Klabu hiyo iliweza kurudi katika Ligi ya Premier ya England na kutimiza mechi 12 bila kushindwa katika msimu wa 2009/10 akiweka rekodi ya klabu hiyo.

Haki miliki ya picha Reuters (audio)
Image caption McLeish afanikisha ushindi

Hatimaye McLeish aliweza kuiongoza klabu hiyo hadi kufikia yeye binafsi alichotaja kama mafanikio makubwa kwake mnamo mwezi febuari 2011, kwa kuibwaga Arsenal katika fainali ya Kombe la Carling 2 -1 ushindi ambao unaipa fursa Birmingham kushiriki michuano ya vilabu barani Ulaya.