Newcastle yamsajili Marveaux

Newcastle imemsajili kiungo cha kati Sylvain Marveaux kutoka klabu ya Ufaransa ya Rennes.

Marveaux amekubali kutia saini mkataba wa miaka mitano.

Haki miliki ya picha skysport
Image caption Ni kati ya wachezaji raia wa Ufaransa waliosajiliwa na Newcastle katika dirisha la usajili la hivi sasa

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 pia alikuwa akiwindwa na Liverpool, lakini sasa atakamilisha utaratibu wa kucheza katika uwanja wa St James' Park, kwa kiwango cha fedha ambacho hakijatajwa.

Utaratibu huo wa kumsajili unatazamiwa kukamilika kufikia tarehe mosi Julai.

Meneja wa Magpies (jina la utani la Newcastle), Alan Pardew, amesema: "ni juhudi kubwa kumpata Sylvain, ambaye amevivutia vilabu kadha.

"Pengine mashabiki wetu wengi hawamfahamu vyema, lakini ni mchezaji ambaye tumekuwa tukimtizama kwa muda."

Marveaux ni raia wa tatu wa Ufaransa kusajiliwa na klabu ya Newcastle hivi majuzi baada ya Hatem Ben Arfa na Yohan Cabaye.

Tangazo la kumsajili mchezaji huyo pia limetolewa siku moja tu baada ya klabu ya Magpies kutangaza pia imemsajili mshambulizi wa kimataifa kutoka Senegal, Demba Ba.

Marveaux atasaidia kujaza pengo ambalo liliachwa na nahodha wa Newcastle, Kevin Nolan, ambaye siku ya Alhamisi alijiunga na klabu iliyoshuka daraja kutoka ligi kuu ya Premier, West Ham.