Mabingwa Man Utd kufika West Brom

Mabingwa wa ligi kuu ya Premier ya England, Manchester United, wataanza kuutetea ubingwa wao kwa kucheza ugenini dhidi ya West Bromwich Albion, katika siku ya kwanza ya msimu mpya, Jumamosi, tarehe 13 Agosti.

Arsenal nayo itaanza mechi yake ugenini pia, dhidi ya Newcastle, huku Chelsea, waliomaliza ligi katika nafasi ya pili msimu uliopita, wakisafiri hadi klabu ya Stoke.

Liverpool watachezea uwanja wa nyumbani wa Anfield, watakapoikaribisha Sunderland.

Swansea itacheza mechi yake ya kwanza ya ligi kuu ya Premier ugenini, dhidi ya Manchester City, huku wageni QPR nao wakiwapokea wachezaji wa Bolton.

Norwich, ambao wamerudi tena katika ligi kuu ya Premier baada ya miaka sita, watasafiri kucheza na Wigan.

Image caption Wanaanza kuutetea ubingwa kwa kucheza ugenini dhidi ya West Brom

Katika viwanja vingine, Tottenham itaikaribisha Everton katika uwanja wa nyumbani wa White Hart Lane.

Fulham ikichezea uwanja wa nyumbani wa Craven Cottage nayo itaipokea Aston Villa, huku Blackburn nao wakiwa ni wenyeji wa Wolves.

Baada ya mechi yake ya kwanza dhidi ya West Brom, Manchester United watakuwa nyumbani Old Trafford katika mechi zitakazofuatia, dhidi ya Tottenham na Arsenal.

Kati ya timu ambazo zilimaliza msimu katika nafasi ya nne bora, mechi dhidi ya Arsenal bila shaka inatazamiwa kuitoa Manchester United jasho.

Mara baada ya vijana wa Wenger kucheza katika uwanja wa St. James Park, watacheza uwanja wa Emirates dhidi ya Liverpool, kabla ya kuelekea kucheza uwanja wa Old Trafford dhidi ya Man United.

Mchezo kati ya Liverpool na Sunderland unamaanisha kwamba Jordan Henderson, mchezaji wa Liverpool, aliyesajiliwa mapema mwezi huu katika mapatano ya pauni milioni 20, huenda akaanza kuitatiza mara moja timu yake ya zamani.