APR yailaza Port Djibouti 4-0

Michuano ya soka ya klabu bingwa kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, ilianza jana mjini Dar es Salaam, Tanzania kwa mechi mbili kuchezwa.

Yanga na El-Merreikh zimetoka sare ya 2-2 huku APR ikiwalaza Port of Djibouti magoli 4-0.

Mechi ya kundi B kati ya Yanga ya Tanzania na El-Merreikh ya Sudan imekuwa mechi ya pekee leo uwanja wa Dar es Salaam, huku mabingwa watetezi APR ya Rwanda pia wakicheza mechi yao ya kwanza siku ya Jumapili dhidi ya Port of Djibouti katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Walikuwa ni El Mereikh waliokuwa wa kwanza kufunga katika dakika ya kwanza kipindi cha kwanza goli lililofungwa na Badru Eldin.

Baadaye Yanga walipata goli la kusawazisha baada ya El Mereikh kujifunga wenyewe na ndipo katika dakika 40 kipindi cha kwanza Yanga wakapata goli pili lililofungwa na mshambuliaji waliyemnunua kutoka Ghana Kenneth Asamoah. Katika kipindi cha pili timu zote ziliingia uwanjani zikiwa na shauku ya kupata ushindi ambapo zilishambuliana kwa zamu na katika dakika ya 87 El Merreikh walipata goli la kusawazisha lililofungwa na Ahme Albasha hadi filimbi ya mwisho zilitoka sare ya 2-2.

Zanzibar Ocean, Jumamosi ilianza vyema kampeni yake ya kushindania Kombe la Kagame, kwani katika mechi ya ufunguzi, ilifanikiwa kuishinda Etincelles ya Rwanda magoli 3-2, katika uwanja wa taifa mjini Dar es Salaam, Tanzania.

Hiyo ilikuwa ni mechi ya kundi A.

Mabingwa wa zamani Simba ya Dar es Salaam walianza mashindano ya Kombe la Kagame bila kufungana mabao na Vital'o ya Burundi, mchezo uliokwisha 0-0.

Image caption Chini ya kocha kutoka Uganda Moses Basena Simba inatumaini kufanya vyema nyumbani

Ijapokuwa Simba wamewahi kuwa mabinga mara saba, ikiwa ni pamoja na mashindano ya kwanza katika uwanja wa Uhuru mwaka 1974, Vital'o walitazamiwa na wengi kujipata katika hali ngumu, kwani wana wachezaji wa umri mdogo, na hawajawahi kutwaa kombe hilo katika historia ya mashindano hayo.

Simba baada ya kuwavunja moyo mashabiki wao kutokana na kudorora katika mashindano ya barani Afrika, sasa itabidi kuwaridhisha wafuasi wao kwa kuonyesha umahiri wao katika mashindano hayo ya Kombe la Kagame.

Kocha wa Simba, Moses Basena kutoka Uganda, itabidi afanye juu chini kuonyesha hamu ya timu yake kuondoka na kombe hilo.

Kwa upande wa mechi za Jumapili, Yanga, Young Africans, pia ya Tanzania bara, katika uwanja huohuo siku ya Jumapili watapambana na El-Merreikh ya Sudan.

Mechi hii ya kundi B inatazamiwa kuwa ni kivutio kikubwa kwa mashabiki, kwani wengi wataikumbuka fainali ya mwaka 1986, ambapo Yanga ikichezea nyumbani, ilishindwa kupiga mikwaju ya penalti ya sawasawa, na hiyo basi kufungwa katika fainali.

Mabingwa watetezi APR ya Rwanda pia watacheza mechi yao ya kwanza siku ya Jumapili, watakapokutana na timu ya Port of Djibouti katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Jumla ya timu 13 zinashiriki katika mashindano hayo, na kuna dola 60,000 za kushindaniwa, senti ambazo zimetolewa na rais Paul Kagame wa Rwanda.

Timu itakayopata ushindi katika fainali itaondoka na dola 30,000.