Kombe la Dunia la kina dada

Mataifa ya Nigeria na Equatorial Guinea yataliwakilisha bara la Afrika katika mashindano ya kina dada ya Kombe la Dunia, yatakayoanza nchini Ujerumani, Jumapili.

Nigeria imefuzu na kuwakilishwa katika kila makala ya mashindano hayo ya Kombe la Dunia kwa wanawake, lakini Equatorial Guinea itashiriki kwa mara ya kwanza.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Nahodha wa Super Falcons ana imani wachezaji wake watafanya vyema Ujerumani

Nigeria itakutana na wenyeji Ujerumani, ambao pia ni mabingwa watetezi.

Vile vile Nigeria itacheza na Canada na Ufaransa katika kundi A.

Equatorial Guinea itakutana na Brazil, Norway na Australia katika kundi D.

Licha ya kucheza katika fainali zote za kina dada, tangu mashindano yalipoanzishwa mwaka 1991, timu ya kina dada ya Nigeria, Super Falcons, iliweza kuvuka mechi za makundi mara moja tu; katika mashindano ya Marekani mwaka 1999.

Mwaka huu Nigeria ina kikosi cha wachezaji tosha, licha ya wengi kushangazwa kwa Cynthia Uwak kukosa kuitwa kujiunga na kikosi hicho.

Mchezaji mzoefu Perpetua Nkwocha, mchezaji aliyefunga magoli mengi zaidi katika mashindano ya kina dada ya Afrika, African Women Championship (AWC) mwaka jana nchini Afrika Kusini, atacheza kando ya Ebere Orji, ambaye aliiwezesha Nigeria kufika fainali ya mwaka 2010 ya vijana chini ya umri wa miaka 20 katika mashindano ya kina dada ya Kombe la Dunia.

Timu ya Super Falcons imekuwa ikifanya mazoezi yake nchini Austria, na hivi majuzi ilitoka sare ya 2-2 dhidi ya Uswisi.