Warner ajiuzulu nyadhifa zote za soka

Makamu wa Rais wa FIFA Jack Warner, ambaye kabla ya hapo alitishia kutiririsha mengi kuhusu jinsi soka inavyoendeshwa, kisha akajiuzulu leo na kupelekea uongozi wa FIFA kumuondolea madai yote yaliyomkumba.

Image caption Jack Warner

Warner ambaye alisimamishwa ili kusubiri upelelezi wa Kamati ya nidhamu ya shirika hilo kuhusu rushwa amejiuzulu kutoka nyadhifa zote zenye uhusiano na soka ikiwa ni pamoja na Rais wa shirikisho la CONCACAF.

Kufuatia uwamuzi wa Warner, FIFA limetowa taarifa kuwa limesikitishwa na hatua yake na kuongezea kuwa kutokana na hilo kamati ya nidhamu inasimamisha upelelezi wote uliokuwa ukifanywa na kuondoa madai yote na kwamba linemuacha kama asiye na hatia.

Warner alikuwa kifanyiwa uchunguzi kuhusiana na ile kashfa ya hongo ya fedha taslimu kununulia kura kwa ajili ya mgombea aliyetaka kuchukuwa mahala pa Rais wa FIFA, Mohammed Bin Hammam.

Kufuatia mtikisiko uliozuka kufuatia kashfa hiyo, Bin Hammam alijiondoa kwenye kinyanganyiro na hivyo kumuacha Sepp Blatter kama mgombea pekee.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bin Hamam aliyejiondoa

Kwa takriban miaka 30 Warner amekuwa mshirika mkuu wa Blatter ambapo Warner kutoka Trinidad alihusika mno na FIFA pamoja na CONCACAF, Shirika linaloongoza soka eneo la Amerika ya Kaskazini, kati na Caribbean. Inafahamika kuwa Blatter alimpa ruhusa Warner kuendesha shirika hilo la CONCACAF anavyotaka ikiwa ataweza kumkusanyia rundo lote la kura kutoka wanachama wote.

Aliposimamishwa hivi karibuni, Warner alitishia kufungua wimbi la ''Tsunami'' juu ya jinsi Soka inavyoendeshwa kupitia mawasiliano yake na Sepp Blatter.

Baadaye aliondoa vitisho vyake kwa misingi kwamba kisheria hangeweza kuanika yaliyokuemo katika mawasiliano baina yake na Blatter.

Kujiuzulu kwake kumekubaliwa na FIFA pamoja na kuusifu mchango wake kwa mchezo wa soka kimataifa.

Kwa wakati huu shirikisho la CONCACAF linaandaa mashindano ya soka ya Mataifa ya eneo hilo ya Gold Cup.