Gervinho afanya majaribio Gunners

Hatimaye klabu ya Arsenal imefikia tamati ya usajili wa mshambuliaji mpya baada ya mda wa maandishi mengi magazetini, sasa baada ya kukamilisha utaratibu wa kuchunguza afya yake na kufikia makubaliano baina ya klabu yake na Arsenal kwa kitita cha pauni za Uingereza milioni £11.2 Arsenal itamtangaza rasmi Gervinho kuwa mchezaji wake .

Haki miliki ya picha 1
Image caption Gervais Yao Kuasi

Mchezaji huyo kutoka Ivory Coast atatangazwa kesho baada ya mwezi mzima wa mvutano na mabingwa wa Ufaransa Lille waliobadili msimamo na kutaka waongezewe kitita lakini sasa inasemekana kuwa atajiunga na kikosi tayari kwa ziara ya bara Asia wiki kesho.

Katika juma ambapo mmoja wa wachezaji waliotia fora msimu wa mwaka 2004 amehama, kukiwa na tetesi kuwa Samir Nasri na Cesc Fabregas watamfuata Gael Clichy, kuna habari njema kwa mashabiki wa Arsenal kuwa mmoja wa washambuliaji mahiri katika Ligi za Ulaya anajiunga na klabu yao.

Akizungumza wiki iliyopita, Gervinho alisema kuwa ''Najiunga na Arsenal kwa sababu ni kikosi cha vijana wadogo na nitaweza kushirikiana nao kwa urahisi. Na kuna uwezekano mkubwa wa kipaji changu kukuwa zaidi.

Kivutio kikuu kwa Gervinho kujiunga na Arsenal ilikuwa kushiriki michuano ya Ligi barani Ulaya na hilo siwezi kulikosa nikiwa na Arsenal, alisema Gervinho ambaye jina la kuzaliwa ni ''Gervais Yao Kuasi''.

Gervinho ni mchezaji wa pili kusajiliwa na Arsenal baada ya Carl Jenkinson kutoka klabu ya daraja la chini Charlton na vilevile Timu ya Taifa ya vijana wenye umri ulio chini ya miaka 19 ya Finland.

Image caption Kocha Arsene Wenger

Meneja Arsene Wenger anatazamiwa kuwaondoa baadhi ya wachezaji wake wa ziada kama Denilson na Nicklas Bendtner kabla ya msimu mpya.

Habari zilizothibitishwa mapema leo ni kwamba Arsenal imemkosa mcheza kiungo kutoka Argentina, Ricky Alvarez baada ya Inter Milan kukubali kulipa kitita sawa na pauni milioni £10.6 ambazo klabu yake ya Velez Sarsfield ilitaka.

Akijiandalia uwezekano wa kuwapoteza Nasri na Fabregas, Wenger anatarajiwa kusajili ma-beki wa hapa hapa Uingereza ikiwa jicho lake linatizama huko Birmingham kumsajili Scott Dann na huko Bolton kuna tetesi kuhusu Gary Cahill.

Halikadhalika kufuatia habari za kumkosa kiungo Alvarez, Wenger ametegea mchezaji mwingine Thiago Motta kutoka Inter Milan, Kocha huyo anahisi kwamba kuwasili kwa Alvarez huko Inter kutamkosesha raha Motta na huenda akavutiwa na mwito wa kujiunga na Arsenal.

Wakati huo huo, klabu ya Arsenal imesema haitotikiswa na hizo pauni milioni 25 kumuuza mcheza kiungo wake Samir Nassir, hilo likiwa jibu la Arsene Wenger kwa wakuu wa Manchester city waliokuja na pauni milioni 19 kwanza kabla ya Chelsea kutishia kitita kikubwa zaidi ya hicho na Manchester united kutangaza kuwa inamtaka kiungo huyo.