Yanga yatinga robo fainali

Timu ya Yanga ya Tanzania leo hii imejihakikishia kucheza hatua ya robo fainali ya Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kagame Cup, baada ya kuisambaratisha timu ya Bunamwaya ya Uganda kwa jumla ya magoli 3 - 2 katika mchezo wa kundi B uliochezwa katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam Tanzania.

Image caption Young Africans

Yanga imeingia robo fainali baada kufikisha pointi 7 huku ikifuatiwa na Bunamwaya yenye pointi 6 pamoja na kukubali kipigo hicho nayo inaingia robo fainali ya mashindano hayo. Al Mereikh yaitwanga Elman Katika mchezo mwingine uliochezwa katika uwanja huo huo wa Taifa Dar es Salaam Al Mereikh ya Sudan imesambaratisha Elman ya Sudan kwa jumla ya magoli 3 - 0. Japo Al Mereikh imeshinda mechi ya leo lakini itabidi kusubiri hadi mwisho ili kujua kama inaweza kupendekezwa kucheza hatua ya robo fainali kama matokeo yake yatakuwa ni mazuri kuliko timu nyingine zilizokosa kuingia hatua ya robo fainali. St.George yaichukiza Port Nako katika uwanja wa Jamuhuri uliopo mkoani Morogoro timu ya St. George ya Ethiopia leo imeinyeshea mvua ya magoli timu Port ya Djibout kwa kuitandika bila huruma magoli 7 - 0 katika mechi ya kundi C na hivyo kuingia moja kwa moja hatua ya Robo fainali ya mashindano ya CECAFA, Kagame Cup. Ulinzi Mbali na St.George timu nyingine iliyojihakikishia kuingia hatua ya robo fainali kutoka kundi C ni Ulinzi ya Kenya ambayo leo imecheza na APR na matokeo yalikuwa sare ya 0-0. Simba kutafuna Red Sea Siku ya Jumapili kuna mechi mbili za kundi A kumalizia hatua ya makundi ambapo Simba ya Tanzania itacheza na Red Sea ya Eritrea na mchezo mwingine utakuwa ni kati ya Zanzibar Ocean View na Vital'o ya Burundi.