Kamati ya Ufundi ya Cranes kuhojiwa

Uwanja wa Luanda Haki miliki ya picha Getty
Image caption Uganda ilishindwa na Angola katika uwanja huu uliotumiwa katika Kombe la Mataifa ya Afrika 2010

Timu ya Taifa ya Uganda iliyosafiri kuelekea Angola ikihitaji kutoka sare kabla ya mechi yake ya mwisho dhidi ya Harambee Stars ya Kenya ilipewa wakati mgumu na mwenyeji wake mjini Luanda katika kipindi cha pili mshambuliaji Manucho akifunga bao la kichwa baada ya kupokea mpira kutoka kwa Djalma mnamo dakika ya 57.

Kama kujibu dua za msikilizaji mmoja kutoka Nairobi aliyeitakia Angola ushindi dhidi ya Uganda ili Harambee Stars iweze kuinyuka Uganda nyumbani kwake mjini Kampala katika mechi ya mwisho.

Hadi dakika za mwisho matumaini ya Waganda yalididimizwa dakika tano za mwisho Flavio alipowazunguka mabeki wa Uganda Cranes na kuipatia Angola bao lake la pili.

Hivyo basi Angola inahitimisha pointi tisa, moja nyuma ya Uganda inayoongoza kwa pointi kumi. Matumaini ya kufuzu baada ya mechi ya Angola yamekwama na sasa itabidi wautumie uwanja wa nyumbani vilivyo watakapoipokea Harambee stars uwanja wa Mandela kule Namboole.

Kufuatia matokeo hayo sasa Kamati ya ufundi ya Uganda Cranes itakabiliwa na masuali juu ya mipango yao ya kuweka kambi ya mazoezi mjini Nairobi.

Hii ni kwa sababu kamati hiyo ilishindwa kufuata utaratibu unaotakiwa chini ya ushauri wa FIFA kuwa Timu ifanye mazowezi mahali ambapo kuna mazingira sawa na yale ya uwanja ambako pambano litafanyika, halikadhalika Timu hiyo hupewa fursa ya kujaribu uwanja huo wakati ule ambapo mechi itachezwa ili kuwapa fursa wachezaji waridhike kimwili na kisaikolojia.

Katika mechi nyingine zilizochezwa Jumapili, matokeo yalikuwa hivi;

Comoros v Zambia 1-2 Bukini v Nigeria 0-2 Zimbabwe v Liberia 3-0 Burundi v Benin 1-1 Jamhuri ya Afrika ya Kati v Morocco 0-0 Niger v Afrika Kusini 2-1 Congo Brazzaville v Sudan 0-1