Mutola aiwakilisha Msumbiji katika soka

Maria Mutola, mwanariadha maarufu kutoka Msumbiji aliyesifika sana katika mbio za mita 800, na ambaye zamani alikuwa akicheza soka kabla ya kuingia katika riadha, amerudi tena katika soka.

Image caption Maria Mutola kutoka Msumbiji ni kati ya wanariadha waliofanikiwa zaidi barani Afrika katika mbio

Akiwa mtoto, Mutola alikuwa akicheza soka na wavulana, kwani wakati huo ligi, wala timu za wasichana, hazikuwepo.

Mutola, maarufu kama 'Maputo Express', baada ya kustaafu kutoka riadha, anaelezea kwamba aliamua kurudi tena katika soka ili kuuweka mwili wake katika afya nzuri, na vile vile kujifurahisha.

Mutola ameelezea kwamba amekuwa akicheza kandanda katika klabu ya Sundowns huko Afrika Kusini, wakati timu ya taifa ya kina dada ya Msumbiji ilipomwita nyumbani ili kuichezea timu hiyo changa ya wanawake katika mashindano ya mataifa ya Afrika yanayoendelea mjini Maputo.

"Kandanda sio mchezo mpya kwangu. Kabla kuingia katika riadha nilikuwa nikicheza soka", alimuelezea mwandishi wa BBC wa habari za michezo, Farayi Mungazi, katika mashindano hayo ya Maputo.

"Kurudi katika soka ni sawa na mtu anayerudi nyumbani, kwani baada ya mazoezi, nahisi mambo yanakwenda barabara", aliongezea.