Man U haiachi tamaa ya magoli

Manchester United ilijaribu kuichapa Bolton, sawa na yale iliyoifanyia Arsenal, kwa kupata ushindi wa magoli 5-0, ikicheza ugenini katika uwanja wa Reebok.

Bolton walikuwa ni wenyeji wa Man U katika mechi ya mwisho siku ya Jumamosi, na ikiwa tayari timu za Arsenal, Man City, Stoke, Tottenham na Chelsea zikiwa zimepata ushindi, kwa hiyo Man U wakawa na hamu kubwa ya kuendelea kuwa kileleni kwa wingi wa mabao.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rooney haachi kutesa msimu huu

Ole wao Bolton.

Wayne Rooney alipata magoli yake matatu, 'hat-trick', huku mchezaji mwenzake Javier Hernandez akifunga mara mbili, na ilikuwa wazi kwamba Bolton walizidiwa nguvu vibaya mno.

United walianza vyema tangu mwanzo, kwani Javier Hernandez alifunga bao katika dakika ya tano ya mchezo.

Rooney alipokea mpira kutoka kwa Phil Jones, na akaongezea bao la pili.

Muda mfupi baadaye, Jones alitimka kana kwamba yumo katika mbio za mita 100, na Rooney alipoupata mpira kutoka kwake, hakusita kutia wavuni bao la tatu katika mechi hiyo.

Hernandez aliongezea la nne, kabla Rooney kupachika wavuni bao lake la tatu.