Majirani Kenya wazima mipango ya Uganda

David Obua
Image caption Mashabiki wengi wanahisi kwamba kama Obua angelicheza pengine ndoto ya Uganda ingelitimia

Angola siku ya Jumamosi iliweza kufuzu kuingia fainali za soka Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012 katika mataifa ya Equatorial Guinea na Gabon, baada ya The Cranes ya Uganda, ikicheza na majirani Harambee Stars ya Kenya, kumaliza mechi yake Kampala kwa kutofungana mabao.

Wachezaji sita hivi walijiangusha chini uwanjani kwa kutoamini wameshindwa kupata ushindi katika mechi hiyo ili kufuzu, huku wengine walielekea chumba cha kubadilishia mavazi wakitiririkwa na machozi.

Baadhi ya mashabiki wa Uganda wanaamini kwamba kama mchezaji wa The Cranes David Obua, ambaye alifukuzwa kutoka kambi ya Uganda, kama angelicheza, pengine matokeo yangelikuwa tofauti.

Waliofurahi ni mashabiki wa Kenya, ambao walionekana wakiwa na mabango ambayo yaliwafanyia dhihaka, kama kuelezea "Ni kweli Uganda haijafanikiwa kufuzu kuingia fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika miaka 34".

Katika viwanja vingine, Niger ilifuzu licha ya kufungwa magoli 3-0 na Misri.

Wapinzani katika kundi G, Afrika Kusini au Sierra Leone wangeliweza kufuzu, lakini katika mechi iliyochezwa katika uwanja wa Nelspruti, ilikwisha 0-0.

Nigeria pia ilishindwa kufuzu, baada ya sare ya 2-2 dhidi ya Guinea katika mechi ya mjini Abuja.

Timu ya Syli Nationale imefuzu kwa kuongoza katika kundi B.

Zambia imefuzu licha ya mechi kumalizika 0-0 ilipocheza na Libya katika uwanja wa Chingola.

Chipolopolo ilihitaji pointi moja tu kufuzu, huku wapinzani wao wa Afrika Kaskazini wakihitaji kupata ushindi ili kufuzu.

Tunisia ilifuzu kwa kuibwaga Togo 2-0 mjini Tunis.

Ghana, ambayo ilifika hadi robo fainali katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010, ilifanikiwa kuingia fainali za Afrika kwa kuishinda Sudan magoli 2-0 katika mechi ya mjini Khartoum.

Cameroon waliishinda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo magoli 3-2 katika mechi ya Ijumaa, lakini cha kusikitisha ni kwamba hawakufanikiwa kufuzu, kwani wanamaliza mechi za kufuzu kwa kushikilia nafasi ya pili, nyuma ya Senegal, ambao tayari wamefuzu, na Jumapili wanacheza na Mauritius.