Uingereza yakomboa meli iliyotekwa

Meli za kivita za Uingereza na Marekani zimeikomboa meli ya Italia kutoka kwa maharamia wa Kisomali, baada ya mabaharia waliotekwa kutuma ujumbe wa kuomba msaada, amesema waziri wa ulinzi wa Italia.

Ignazio La Russa amesema mabaharia 23 walikuwa wamejifungia ndani ya chumba ndani ya meli hiyo ya mizigo iitwayo Montecristo.

Meli hiyo ilitekwa nyara kilomita 1000 kutoka pwani ya Somalia siku ya Jumatatu.

Jeshi la Uingereza halikupata upinzani wowote wakati walipokwenda kukomboa meli hiyo na kuwakamata washukiwa 11 wa uharamia, wamesema maafisa wa wizara ya Ulinzi ya Uingereza.

Wizara ya mambo ya nje ya Italia imesema "imefurahishwa sana" na hatua ya uokoaji, na kusema mabaharia wa meli hiyo, saba wa Italia, 10 kutoka India na sita kutoka Ukraine wapo katika hali nzuri.