Mbunge wa Nigeria 'auliwa na Boko Haram'

Polisi wa kaskazini mwa Nigeria wamesema watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kundi la kiislamu wamempiga risasi na kumwua mbunge mmoja.

Watu hao waliokuwa na bunduki walimpiga risasi na kumwua Modu Bintube nje ya nyumba yake mjini Maiduguri, katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Kundi la Boko haram limekuwa likilaumiwa kufanya mashambulio kadhaa katika miezi ya hivi karibuni, mara nyingi wakiwalenga maafisa wa serikali.

Watu wanne pia wameuawa kutokana na mlipuko wa bomu katika mji mkuu wa jimbo la Gombe.