Kenya yamuita balozi wa Eritrea

Kenya imemuita balozi wa Eritrea nchini humo kutoa maelezo zaidi kuhusu madai kwamba Eritrea inawapa msaada wa silaha wapiganaji wa Al Shabaab.

Balozi Beyene Russom amekutana na waziri wa masuala ya kigeni wa Kenya Moses Wetangula mapema leo asubuhi katika mkutano ambao umesemekana kuwa na majibizano makali.

Kenya imetoa ushahidi wa kijasusi unaonyesha kuwa Eritrea inawapa silaha wapiganaji wa Al Shabaab. Inadaiwa ndege mbili za kijeshi zilizosheheni silaha zilitua katika maeneo yanayodhibitiwa na Al Shabaab

Balozi wa Eritrea amekanusha madai hayo na kuahidi kwamba waziri wa masuala ya kigeni wa nchi hiyo atazuru Kenya wiki ijayo kuweka mambo bayana.