Wanajeshi waasi waongezeka Syria

Idadi ya wanajeshi waasi imeanza kuongezeka nchini Syria huku visa vya jeshi la nchi hiyo kushambuliwa vikiongezeka. Hata hivyo idadi hiyo ya waasi ni ndogo sana hivi kwamba wao pekee hawawezi kukabiliana na kupindua Serikali ya nchi hiyo.

Kundi hilo la waasi linalojiita Free Syrian Army linasema kuwa lina karibu wanachama 15,000 walioasi jeshi la Serikali. Wengi wanaona kuwa takwimu hizi zimetiwa chumvi.

Jeshi la Syria lenyewe lina askari 200,000 na kurutu idadi sawa na hiyo. Wanajeshi wengi hata hivyo hawajatikisika katika imani yao kwa Rais Assad. Idadi kubwa ya wanajeshi walioasi wanasema kwamba wamefanya hivyo kwa sababu hawangekubali kuwafyatulia risasi watu wao.

Mji wa Homs na mji wa Kusini wa Deraa ndiko kuna wanajeshi waasi wengi zaidi. Wanasema kuwa lengo lao ni kuwalinda waandamanaji. Hata hivyo kundi hilo limekuwa likiwashambulia wanajeshi wa Serikali mara kwa mara.