Mfalme wa Morocco amchagua waziri mkuu

Mfalme Mohammed wa Morocco, amemteua kiongozi wa chama cha Kiislamu ambacho kimeshinda uchaguzi wa wiki iliyopita kuwa ni waziri mkuu.

Abdelilah Benkirane ambaye ni mkuu wa chama cha Haki na Maendeleo, amekula kiapo cha kuwa mtiifu na ataanza mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano.

Chama hiki hakijawahi kuwa serikalini, lakini kimepata ushindi mkubwa sana katika uchaguzi wa wabunge wa siku ya Ijumaa.

Chini ya katiba mpya iliyobuniwa mwezi Julai ilishinikizwa na umma kuwa mfalme lazima amchague waziri mkuu kutoka katika chama kilichopata viti vingi kwenye uchaguzi.