Marekani yataka Iran imwachie aliyekiri

Marekani imetoa wito kwa Iran kumwachilia huru ‘bila kuchelewa’ raia wa Marekani mwenye asili ya Iran ambaye Tehran inamwita ‘jasusi’ wa shirika la Kijajusi la CIA.

Amir Mirzai Hekmati alikiri kupitia televisheni ya Taifa kuwa alitumwa kupenya na kuingia katika taasisi ya upelelezi nchini Iran.

Msemaji wa serikali aliiambia BBC kuwa Marekani imeomba kuonana na Bw Hekmati kupitia ubalozi wa Switzerland, unaofanya kazi kama mpatanishi kati ya nchi hizo.

Familia yake imekanusha kuwa mtoto wao alihusika na upelelezi.

"Mwanangu si jasusi. Hana makosa yoyote. Ni kijana mzuri tu, raia mwema na mtu mzuri," Ali Hekmat aliambia shirika la habari la ABC. "Ni tuhuma ambazo hazina msingi wowote na rundo la uongo."