Maafa mjini Baghdad

Wizara ya afya katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad inasema milipuko ya mabomu imesababisha vifo vya 40 na kujeruhi wengine wengi.

Wizara ya mambo ya ndani imeiambia BBC kuwa mashambulio hayo yametokea katika maeneo kumi na matatu.

Maeneo tofauti ya mji huo yamelengwa. Katika siku za hivi karibuni, mzozo wa kisiasa nchini Iraq umeendelea kutokota huku kukiwa na hali ya wasiwasi kati ya viongozi wa Kishia na Sunni.

Mzozo huo ni kuhusu kibali cha kumtia nguvuni makamu wa rais wa Kisunni Tariq al-Hashemi.

Mashambulizi hayo yameibua maswali kuhusu maafisa wa usalama wa Iraq na iwapo wako tayari kulinda nchi baada ya kuondoka kwa jeshi la Marekani mapema wiki hii.