Ravalomanana wa Madagascar atarejea?

Rais wa zamani wa Madagascar Marc Ravalomanana ambaye amekuwa akiishi uhamishoni nchini Afrika kusini tangu alipoondolewa madarakani amesema atarejea nyumbani siku ya Jumamosi.

Maafisa wa usalama wa Madagascar wamesema akiingia nchini atakamatwa.

Bw Ravalomanana aliondolewa madarakani kwa nguvu na Andry Rajoelina akisaidiwa na jeshi la nchi hiyo mwaka 2009.

Tangu wakati huo kumekuwa na juhudi kadhaa za kupata ufumbuzi wa kisiasa lakini imeshindikana.

Bw Ravalomanana ameshitakiwa akiwa hayupo nchini kwa njama za kufanya mauaji wakati wa fujo zilizosababisha apinduliwe lakini yeye amesema mahakama haikuwa ya halali.