Kifo cha Mujuru: 'Polisi alilala'

Uchunguzi juu ya kifo cha aliyekuwa mkuu wa majeshi wa Zimbabwe Solomon Mujuru umebaini polisi aliyekuwa zamu alikuwa kalala wakati moto uliomwuua ulipoanza.

Baada ya kuamka, polisi huyo alisema alishindwa kupata msaada kwasababu simu yake iliisha salio na redio yake ilikuwa haifanyi kazi.

Uchunguzi huo pia uliambiwa kwamba gari la zima moto lilipofika kwenye shamba hilo, halikuwa na maji ya kuzima moto huo.

Jenerali Mujuru alikuwa miongoni mwa wanasiasa waandamizi wa Zimbabwe na alikuwa amemwoa Makamu wa Rais wa nchi hiyo Joice Mujuru.