China yaionya Marekani

Shirika la habari la serikali ya China limeionya Marekani dhidi ya "kutunisha misuli yake" baada ya Marekani kuzindua mpango wa ulinzi unaoelekeza mtazamo wake eneo la Asia-Pasifiki.

Maoni ya mhariri ya shirika hilo la Xinhua, yamesema hatua ya Rais Barack Obama kuongeza wanajeshi wake katika eneo hilo huenda kukapokelewa kama ishara ya uimara na amani.

Lakini pia shirika hilo limesema jeshi la Marekani huenda likahatarisha "hali ya amani".

Bw Obama anapanga pia kupunguza dola bilioni 450 katika jeshi ili kuunda jeshi "kakamavu" zaidi.

Maelfu ya wanajeshi wanatarajiwa kupunguzwa kazi katika muongo ujao chini ya mabadiliko hayo ya kiusalama.