Mgomo wa kitaifa kuanza Nigeria

Vyama vya wafanyikazi nchini Nigeria vinajitayarisha kuongoza mgomo wa kitaifa hii leo kulalamikia hatua ya serikali kuondoa ruzuku ya mafuta.

Bei ya bidhaa hiyo imeongezeka mara dufu tangu tangazo la serikali kuanza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka huu. Hii ilipelekea maandamano ya nchini kupinga mpango wa serikali.

Maelfu ya wafanyikazi katika sekta za umma na binafsi wanatarajiwa kushiriki mgomo wa leo ambao umetajwa wa kwanza wa kitaifa nchini humo tangu mwaka 2003.

Mwandishi wa BBC mjini Lagos amesema mgomo wa leo huenda ukasambaratisha shughuli nyingi nchini Nigeria.

Raia wengi wa Nigeria wameona ruzuku kama faida ya pekee kutokana na taifa lao kuzalisha mafuta, japo serikali imesema ruzuku hiyo imeathiri vibaya uchumi wa nchi.

Hapo Jumapili katika kikao cha dharura cha bunge, viongozi wa kisiasa wameitaka serikali kutafakari upya hatua ya kuondoa ruzuku hiyo.