Mawaziri wa Yemen wampa kinga rais Saleh

rais Saleh wa Yemen Haki miliki ya picha Reuters

Baraza la mawaziri nchini Yemen limeidhinisha mswada wa sheria mpya inayompa kinga dhidi ya kushtakiwa rais wa taifa hilo Ali Abdullah Saleh pamoja na maafisa waliohudumu katika utawala wake wa miongo mitatu.

Rais huyo ameridhia kuachia ngazi mwezi ujao kwa sharti la yeye au jamaa wake kutoshtakiwa kwa mauaji ya waandamanaji waliopinga utawala wake.

Shirika la utangazaji la kitaifa limesema kinga hiyo imewekewa waliofanya kazi katika serikali ya bw. Saleh ikiwani pamoja na raia, jeshi au polisi.

Mswada huo unasubiri kuidhinishwa na bunge. Katika majuma ya karibuni maelfu ya raia wa Yemen wamekuwa wakiandamana kushinikiza kushtakiwa kwa rais huyo dhidi ya mauaji ya waandamanaji wakati wa maandamano ya miezi tisa.