Kituo cha jeshi chashambuliwa Somalia

Bomu limelipuka kwenye lango kuu la kuingia kwenye kituo cha jeshi la Ethiopia nchini somalia.

Basi lililokuwa limesheheni mabomu liliendeshwa hadi kwenye kizuizi cha bara barani kilichopo mbele ya lango kuu la kituo cha kijeshi cha Ethiopia cha Beledweyne. Askari wa Ethiopia alilifyatulia risasi basi hilo kujaribu kulisimamisha .Hapo ndipo dereva wa basi hilo alipolipua bomu.

Kundi la wanamgambo wa kiislam la Al Shabab, limesema ndilo lililofanya shambulio hilo na kuripoti kuwa takriban wanajeshi 20 wa Ethiopia wameuawa .

Hata hivyo walioshuhudia tukio hilo katika eneo la Beledweyne hawakuthibitisha idadi ya vifo.

Mwezi uliopita vikosi vya Ethiopia viliuteka mji huo ambao ni muhimu uliokuwa ukidhibitiwa n Al Shabab. Katika miezi ya hivi karibuni, wanamgambo wa kiislam wamekabiliwa na mashambulio makali .