Wamiliki wa Costa Concordia kulipa fidia

Wamiliki wa meli moja ya kifahari iliyozama katika pwani ya magharibi ya Italia mapema mwezi huu, wametangaza kuwa wako tayari kuwalipa fidia abiria wote waliokuwa kwenye meli hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti, kila abiria atalipwa dola elfu kumi na tano. Haya yanajiri baada ya majadiliano kati ya mashirika kadhaa ya kutetea maslahi ya wateja nchini Italia.

Fedha hizo ni fidia kwa abiria ambao walipoteza mali yao na pia kuathirika kiakili. Hata hivyo mkataba huu haushirikishi watu waliopoteza jamaa wao katika mkasa huo au wale waliojeruhiwa.

Miili kumi na sita tayari imepatikana kutoka kwa mabaki ya meli hiyo ijulikanayo kama Costa Concordia.

Watu wengine kumi na sita hawajulikani waliko.