Ujumbe wa Kiarabu kwenda Syria

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema jumuiya ya nchi za kiarabu ina mipango ya kurejesha tena wawakilishi nchini Syria na kuwa jumuiya hiyo imeitisha usaidizi wa umoja wa mataifa.

Katibu huyo alisema kwamba mkuu wa jumuiya hiyo Nabil el-Arabi alikuwa amemwambia kuwa alitaka kutuma tena ujumbe wa jumuiya ya nchi za Kiarabu nchini Syria lakini ulikwama kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.

Bwana Ban amesema uamuzi wa serikali za Urusi na Uchina kutumia kura zao za turufu kupinga vikwazo zaidi dhidi ya utawala wa Syria, umeifanya serikali ya nchi hiyo kuimarisha dhuluma dhidi ya raia wake.

Serikali za magharibi kwa sasa zinafatuta njia ya kumaliza mgogoro huo.

Majeshi ya serikali ya Syria yameendelea kushambulia maeneo yanayomilikiwa na vikundi vya upinzani.