Waasi Sudan waomba msaada

Waasi wa SPLM wanaopambana na serikali ya Sudan upande wa kaskazini wa mpaka na Sudan Kusini wamesema hali ya raia ni mbaya zaidi.

Kiongozi wa kundi hilo la waasi wa SPLM -North, Malik Agar, ameiambia BBC kuwa zaidi ya watu 200,000 katika jimbo la Blue Nile wanahitaji usaidizi wa haraka.

Amesema watoto na watu wazee wameanza kufariki na ametoa wito wa kutolewa kwa msaada wa dharura na jamii ya kimataifa.

Kundi hilo la waasi wa SPLM-North limetia saini makubaliano na shirika la Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika kupeleka chakula kwa maeneo yaliyoathirika na mapigano, lakini Bw Agar amesema serikali ya Khartoum imezuia msaada kuingizwa.